Sunday, December 2, 2007

Boyfriend & GirlFriend

Kuishi Pamoja!
...ni kweli kunapoteza nafasi ya ndoa?

Jamani Eeh, ....mwaka umeisha, na kama ulikuwa hujui kabisa, leo ni Desemba moja, ..unaona bwana? Siku ya Ukimwi duniani, hapa nilipo mwenzia nimepima tangu jumatano na niko pa, na miaka hii 32 sasa nahisi kama nioe hivi, ...au mnasemaje majamaa? Nshakuwa mtu mzima bwana ngoja niangalie kushoto na kulia kisha nikae upande wa pili wa mabachela niwe mpinzani wao. Nahisi italeta maana.
Tafakuri yetu ya leo jamani inatokana kama kawaida na ujumbe mwingi ambao huletwa na wasomaji wetu, ...kwa kawaida huwa naangalia wasomaji wengi wameongea kuhusiana na nini? Wengi wao wiki hii wamenogewa na penzi, wanataka kuhakia kwa wapenzi wao, wake kwa waume, tatizo liko kwa akinadada, wanahisi kama wakihamia tu, ndio kuolewa basi maana kutakuwa hamna jipya!
Mnanisoma?
Vijana kama vijana, wamekaa chini na kujadiliana jinsi hizi pesa za kwenda nyumba za wageni zinavyopukutika, au mara huyu kampa huyu hela ya kula wakati wangekuwa nyumba moja wangepika na kula kwa gharama nafuu na ule ukaribu tu wa kushauriana hili na lile ukiwepo pia ni sawa, maana kama kusomana tabia huu ndio muda wake? Lakini sasa, wakinadada wanadai kwambaaaaaa, ukishakaa na mtoto wa kiume, ...kuolewa sahai, anakuchezea kisha akuache. Hii ni kweli?
Au ndio twende kwenye mavipengele mwanawane? Haya twendeni tukaone kwa mtazamo wangu mimi ninavyoliangalia hili, huku nikiendelea kukusihi kwamba, si lazima uamini kila ninalosema mimi kwani na mimi jamani ni binadamu wa kawaida tu ambaye nina mapungufu yangu.
Chuja pumba, chukua nafaka, ...tumeelewana?

1. Kwa nia njema? ...mbona fresh tu!
Kuna kitu kimoja ambacho mimi nakiamini kila siku katika maisha yangu na nina imani kwamba hii ni moja ya imani ambazo nitazeeka nazo. Unanisoma? Penzi huleta mabadiliko makubwa katika maisha ya binadamu kama ulikuwa hujui sasa wewe una nia njema na mwenzako kwa nini uogope? Usafi wa nia huleta mabadiliko kama ulikuwa hujui...
Sasa hapa ujue kuna nini, mtu anaweza akawa kabisa ana nia ya kukuchezea, aishi na wewe kisha akuache lakini kuna moja lipo wazi sana. Mwanamke ukiamua kum'badilisha mwenzako mawazo mbona ni kazi ndogo tu? Huduma zile za baba mwenye nyumba kutoka kwa mama, zitamsahaulisha kila kitu na akitoka kwenye mtego huu huyo kashindikana,, usihangaike naye atakuua!
Anza asubuhi maji ya kuoga, atavaa nini, mchana asikose SMS za kumkumbusha kula kama anafanya kazi jioni akitoka kazini mambo yetu yale kama kawaida, ....nina uhakika, nia njema hujenga njia njema.

2. Hapa ndio penye ukweli...
Ujue bwana sisi vijana wa mjini tuna tabia moja ambayo watu wanahisi ni muhimu na ya kudumu lakini ni mbaya sana ya uongo. Mkianza mapenzi, kila mmoja atamdanganya mwenzako kuhusiana na jambo moja ama jingine si kwa nia mbaya, lakini mara nyingi huwa ni katika kuhakikisha kwamba uhusiano unakaa kwenye mstari, lakini mwisho wa siku, uongo ni m'baya!
Unaona bwana, sasa katika kuhakikisha kwamba mnaishi uhusiano salama, njia njema ya kuujua ukweli ni kuishi pamoja. Mnanisoma? Mkikaa pamoja lolote ulilodanganywa utalijua tu. Na mimi nahisi ni bora ukae miezi mitatu na kuujua ukweli ili kama unajitoa ujitoe kabla mambo hayajawa mabaya kuliko kukimbilia kufunga pingi za maisha halafu unakutana na mambo makubwa ukiwa ndani tayari. Ujue ni balaa?
Watu wakitaka yao huficha makucha bwana, hujifanya kuwa na tabia ambayo ni njema sana kwa sababu tu anataka lake, akishalipata anajisahau sasa, ndio unaanza kusema kabadilika, kumbe alibadilika wakati anakutaka, ...kwa sasa kwa kuwa kashakupata, tabia halisi kabisa ndio inakuja sasa.
Sasa kuliko mtu kukufanyia ujinga akiwa tayari keshakufunga pingu za maisha, ni bora ukazijua tabia zake za kweli ukiwa kama nje ya uwanja, ili ufanye maamuzi sahihi, kama utayavumilia haya, kama unahisi yatakushinda mwaya, ...ni bora ujiepushe mapemaaaaa...

3. Penzi la kweli halichuji!
Kama una penzi la kweli inakuwaje unachokwa? penzi la kweli halichokwi, na watu hawa kama wanajigundua kama wana mapungufu huamua kuambiana ukweli na kurekebishana na sio kuamua kuumizana na mwisho wa siku kuachana. Kwa hiyo kama una penzi la kweli kwa mwenzio ujue kuna uwezekano mkubwa sana wa kudumu.
Tabia hubadilishwa na penzi kaa ulikuwa hujui, nikupe njia, muonjeshe kwanza ule utamu wenyewe mwenzio. Ukiona karidhika sasa, mwambie hutaki hiki, na hiki na kile, ...umeona bwana, atabadilika mwenyewe na mtakuwa sawa.
Mi nakwambia, huna haja ya kuogopa kwamba nikikaa naye penzi litachujuka, kutakuwa hamna jipya, kwamba atakuchoka atakuacha. Wasiwasi wangu ni kwamba huenda akanogewa bwana, mambo yakawa mazuri kiasi mwenyewe ukafurahi.
Jamani, mimi mwenzenu naishia hapa, Krismas ndio inakuja jamani, kuna watu wanasema wao hawana simu kabisa lakini wanataka kuwasiliana na ukurasa huu basi anuani ya posta jamani.
Andika kwa :
Henry Mdimu
Boyfriend & Girlfriend
P.O BOX 19754
Dar es Salaam

Kwa Email ni:
Hmdimu@Mwananchi.co.tz

Kwa SMS
+255 787 000 880

No comments: