
Ukipata ujauzito?
...nini kinafuata?
Kaka na dada zangu natumaini hamjambo na mnaendelea vema na shughuli za ujenzi wa Taifa, wasomaji mahiri kabisa wa ukurasa huu, ahsanteni kwa muda wenu, mimi mzima na maisha ni mafupi kusema ukweli, lakini nitakuwa nakosea nikiacha kuyapa sifa yake, ...matamu!
Shukrani kwa wasomaji wangu wa Zanzibar walioamua kushuka kwenye boti, na kuja moja kwa moja mpaka Tabata Relini kuja kumuona, huyu mwandishi wa makala wanazozipenda, zinazowagusa anafananaje? Walipoondoka kuna neno waliniambia likanifanya niwe mpole kidogo, unajua walisemaje? Hata siku moja, usithubutu kumkadiria mtu kwa kumtazama. Utakuwa umekosea sana!
Haya, tuachane na hizi kazi za Mungu, naomba leo tuangalie mambo makubwa yanayothusu sisi vijana wa kike na kiume wa kiAfrika, nazungumzia suala la ujauzito leo. Mmeamua kuwa mtu na mpenziwe, ikafikia hatua sijui ndio tuseme mlijisahau, au nini, ni kitu gani cha kwanza mtafikiria kufanya? Au huwa mnajihisii nini mkifikia hatua hili likatokea kaka na dada zangu?
Kusema ukweli jamani, mengi hufikiriwa hapa, kuna watu hufikia hatua ya kutoroka hata makwao, wakihofia ukali wa wazazi wao, au wakihofia aibu kwa umma, imani ni kwamba, mimba nje ya ndoa ni dhambi ya uzinzi, ambayo kiukweli jamii ikijua kwamba unaifanya bila haya haya, linaweza kuwa tatizo.
Mimi nina yangu ambayo nayafikiria katika hili, naomba nipewe wasaa nianze kumwaga vipengele vyangu. Si sawa jamani:
1. Sio ajabu, ..kawaida...
Ukweli uko hivi, kile kitendo tu cha kuwa wapenzi, kwa utamaduni yetu wa kiafrika, iko bayana kwamba uhusiano huu unahusisha pia tendo la ndoa, ambalo mwishilio wake ndio huu, hasa mkiwa sio watu wa kutumia kinga ya aina yeyote. Tunaelewana, kwa hiyo kwa kushiriki tendo la ndoa, suala la kupata ujauzito lina uwezekano mkubwa hapo jamani, nadanganya?
Sasa cha ajabu nini hapo? Umepanda mpunga, mchele ndio huo. Aibu inatoka wapi wakati ulikuwa pengine unafurahia, kinachofuata hapo ni jinsi ya kukabiliana na tatizo lenyewe, kama kweli wewe unaliona tatizo. Lakini kusema kwamba sijui hukutegemea, unajidanganya mwenyewe, kwa kuwa asilimia kubwa, ni watu wanaojua wanachokifanya. Na kama ulikuwa huutaki huu ujauzito, mbona hata tahadhari hukuchukua? Uliutaka bwana!
Atakayekucheka pia atakuwa mjinga, maana waliozaliwa nje ya ndoa siku hizi ni wengi kuliko hata waliozaliwa ndani ya ndoa, unatakiwa kujipanga hapa na jinsi ya kukabiliana na tatizo lenyyewe, ni lako na hutakuwa na pa kulikimbiza, ...unalo hilo!
2. Haichochei chochote!
Kuna akinadada bwaba huamini kwamba ukim'bebea mtu mimba basi kuna uwezekano mkubwa akawa ndio wako wa maisha. Naomba kuchukua wasaa huu kuwatahadharisha dada zangu kwamba hili si kweli kwamba kunibebea ujauzito, kunaweza kunihamasisha mimi kukuoa, au labda kuishi na wewe kama mtu na mwenzake,...kwa akili zetu vijana wa siku hizi, unaweza kuwa unanikimbiza. Tunaogopa majukumu kuliko tunavyoyaogopa magonjwa ya zinaa, ...mdio ukweli mdio ,maana sioni aibu kulisema hili kwa watu. Si tunajijua?
Nimelisema makusudi maana wanaolalamika mtaani wako wengi, ya kwamba wamekimbiwa, huamua tu kubeba mimba bila ya kuwaambia wenzao, kisha huwashtukiza. Jamaa sasa mara nyingi sijui ndio kusema hawajajiandaa na maisha ya malezi, hukataa, au kukimbia kabisa mji. Ukiangalia sio busara lakini sasa utafanyaje na ndio ushakimbiwa?
Tunabakia pale pale pa kukubali matokeo na kuangalia nini cha kufanya baada ya yote hayo.
3. Unaua? ...ni dhambi zaidi!
Hili ni kimbilio la wengi, kukimbilia kutoa akiamini kwamba amemaliza tatizo, kumbe ndio anajitengenezea matatizo zaidi maana duniani kama mlikuwa hamjui, ni Mungu ametuleta, amekupa uwezo wa kupata kiumbe, unakiua, unafikiri unamfurahisha? We ngoja matokeo yake, hukumu siku hizi iko hapa hapa duniani kama mikuwa hamjui.
Hii ni ya kiimani zaidi, fikiria umefanya dhambi ya uzinzi, hutosheki nayo unaenda kuua tena, halafu huyu Mungu unamuangaliaje? Baso utamtaka msaada? Bado utasema maisha yako yamekosa baraka na utakuwa unahisi kama unaonewa hivi, jibu mwenyewe kabla hatujafunga kurasa.
Kutoa mimba ni hatari kwa afya, na kwa kweli hata kiimani ni mbaya kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba, kama unahisi kwamba huko tayari jamani kinga mbona zimejaa kibao? Shauriana na mwenzako au kama vipi acha kabisa haya mambo kama huko tayari nayo.
Mimi hapa kwa leo ndipo nahisi niishie, nataka kuwasiliana zaidi na watu wangu mniambie kuhusiana na hili mnaonaje? Niandikieni email:
Mdimu@hotmail.com
Simu:
+255 787 000 880