Hivi, unajituma au unataka kutumikiwa?
Jamani imefika ile jumamosi ambayo kuna watu wengi wananiambia kwamba huwa wanaisubiri sana, eti waangalie nimesema nini leo? Jamani hivi mnajua kwamba sasa hivi nakuwa napata wakati mgumu sana ninapofikiria kufanya jambo? na hii ni kwa sababu kuna watu wengi makini wananisoma kwa sasa.
Shukrani za dhati kwa wasomaji wangu wa Arusha, ..tulikutana bwana tukajadili mengi tu na tulifurahi kwa kweli kuonana, wengi walishani watakutana na jibaaaaba hilo, kumbe kakijana tu lakini wengi wameniombea, kila mtu kwa imani yake kwamba Mungu anijaalie busara zaidi, maana ninayosema huwa hayalingani na umbo langu na miaka niliyonayo, eti wanadai naongea maneno ya kijana mwenye umri wa miaka 40, ...jamani!
Tuendelee na ya leo maana hizi sifa nikianza kuzielezea wala haziishi, ...kaka na dada zangu, nimesukumwa kuandika haya ninayoandika leo, kuna watu wananiandikia malalamiko kila kukicha. lawama kwa wapenzi wao wakidai kwamba hawaoni kama wanapendwa, yaani wenzi wao hao hawajitumi kabisa katika mapenzi, lakini kuna jibu nikawaandikia, ambalo liliwafanya wanyamaze, unajua niliwauliza nini?
Sawa hao wenzenu hawajitumi, na nyie wenyewe, mmeonesha jitihada gani kuwaweka karibu, ama mnataka kutumikiwa? Kwani jamani mapenzi ni kupenda ama kupendana? Maana wewe unasema huoni dalili kutoka kwa mwenzako, wewe zako ulionesha zikawekwa benchi? sasa kuna utaratibu wa kuangalia katika haya mapenzi, hasa kwa wale ambao walifuatwa, na sio wao kufuata, mnatakaiwa kujua mambo flani ambayo nitawawekea katika vipengele. Tupo p amoja jamani? ..me naanza:
1.Mapenzi na kuamua!
Hili ni jambo ambalo wengi wa vijana waliokuwemo katika uhusiano mlikuwa hamjalifahanu basi habari ndiyo hiyo. mapenzi ya kutegeana yamepitwa na wakati na ni kujidhulumu na mwisho wa siku utajikuta huridhiki na kila unayemuona maana utagundua kwamba labda hakuopendi kumbe wenyewe mnategeana na mwisho wa siku mnajikuta mnahisiana vibaya baada ya kila mtu kutegea kumuona mwenzake akiwa kajitoa kwa mwenzake.
Kama umeshaamua kwamba wewe uko na fulani haina kutegea kaka ama dada yangu. Umeamua kupenda, penda moja kwa moja, na hatua ya kwanza katika hili ni kufukia mashimo. Uliza kivipi? Unapoona anakosea rekebisha, unapohisi hupendi mambo fulani, ambayo mwenzako anayafanya, mwambie ukweli, na kwa kuwa yeye anakupenda anajirekebisha, wazungu wanasema, 'Love makes things happen', na mimi nawaunga mkono, nimeshuhudia watu wakiacha pombe, wakiacha sigara, wakiacha hata umbea kwa sababu ya mapenzi.
Lakini ukitega, kila mtu utamuona ana tabia mbaya, na kumbe tabia mbaya unayo wewe. na kibaya zaidi sasa, unajikuta umeachana na huyu, umeanza na huyu, ukaenda kwa huyu na huyu na yule na mwisho wa siku umefanya msuruuuru wa watu katika uhusiano wako wa kimapenzi. Na dunia si unaijua ilivyofunyangwa na teknolojia. Ndio yaleeee, unaingia mahala unakuta katika watu kumi, wanne umeshakaa nao mkao wa kimapenzi? Heshima ipo hao?
Unajinyima mwenyewe uhuru wa nafsi unakuwa, au nadanganya? ...semeni...
2. mapenzi huambatana na amani ya moyo?
Ndio maana hapo mwanzoni nikawaambia kwamba ukiamua kufanya uhusiano amua tu moja kwa moja maana uhusiano wa kuchungulia chungulia unakuwa kama hujiamini hivi, unakuwa na moyo wa kusita sita, kuliko kufanya hivi ni bora kuacha kaka au dada yangu maana hutafurahia, utakuwa kama unajinyima haki yako ya msingi.
Sasa mambo ya kukaa kama bosi na kusubiri mwenzako ahangaike ndio nini. Na yeye kwa kukuona hivyo unataka kusujudiwa unadhani atakubali kufanywa mjinga, na yeye huenda akawa na mtu anamnyenyekea, atahisi kwamba kwako hamna mapenzi. Kumbe yawezekana yamo, ila sasa tatizo ni kwamba, unasikilizia kwamba kama kweli lipo, ...ndio unakuta muda unakwenda, mmoja ataona anayeyushwa, mara uhusiano unabomoka, ...kila mtu kivyake!
Unatakiwa kabla ya kumwambia mtu I love you too, umehakikisha kabisa kutoka moyoni mwako kama umeamua na moyo ukiamua kupenda unakuwa na amani na ule uhusiano ambao unauanza. Unaona bwana na ukipata baraka kutoka moyoni mwako, penzi la namna hii hudumu asikudanganye mtu na ukihisi moyo unasita, achana na huo uhusiano, utakupotezea muda bila mwenyewe kujijua, na kama huniamini jaribu, ..haufiki popote uhusiano wa namna hii.
3.Nyie tu na mambo yenu
Kuna kosa kubwa ambalo vijana hulifanya pindi wanapokuwa katika husiano zao. Hupenda sana mambo mawili, moja ni kupenda sana kushirikisha rafiki zao katika husiano zao, yaani kuanzia kwenye maamuzi ama katika jambo ambalo wenyewe huliita ushauri kumbe wanakuwa wanauza silaha za maisha yao. Kikulacho ki nguoni mwako kama ulikuwa hujui, ..we una uhakika gani huyo unayemuomba ushauri anafurahia maisha yako na mpenzio?
Hili ni moja jingina bwana, ni lile la kulinganisha mambo, kwamba mbona flani anafanyiwa hiki mi sifanyiwi? Maisha ni kama vidole mikononi mwako, hayawezi kulingana, kuna aina ya maisha ambayo Mungu amekupangia, unatakiwa kukubali hali uliyonayo na kuirekebisha kwa zana ambazo ziko ndani ya uwezo wako, unaona bwana? ukilazimisha tu unakuwa umeharibu kila kitu.
Nomba niwashauri kitu kaka na dada zangu, rafiki yako mkubwa awe mpenzi wako, kama kweli unampenda, yeye ndio mshirikishe kwenye mambo yako na mwisho wa siku utakuja kuona, kila kitu kitanyooka, unajua hii itatoka wapi? ...katika kuhakikisha kwamba mnaridhiana.
Umri unaenda mbele ndugu zangu, hili nawaambia kila siku, mnafikiri bado tuna muda wa kupoteza vijana wenzangu? Mangapi yanatusubiri kwa ajili ya maisha yetu ya baadae?
Naomba niishie hapa kwa leo ndugu zangu, nina imani somo mmelipata na kama mna la zaidi la kuniambia, naomba mniandikie kule kwenye:
HMdimu@Mwananchi.co.tz
+255 787 000 880
Wiki ijayo, ...nipo hapa hapa, ..msikose.
No comments:
Post a Comment